11 Desemba 2025 - 13:05
Utawala wa Kizayuni: Hezbollah imerejesha uwezo wake wa kijeshi katika sehemu kubwa ya majimbo ya mapigano (Mapambano)

Maafisa wa Israel wametoa tahadhari kwamba Hezbollah, kwa msaada wa kifedha kutoka Iran, imefanikiwa kurejesha uwezo wake wa kijeshi na sasa inachukuliwa kuwa tishio la kimkakati kwa Tel Aviv.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Gazeti la Yedioth Ahronoth, likinukuu maafisa wa ngazi za juu wa utawala wa Kizayuni, limeandika kuwa Hezbollah imeweza kurejesha sehemu kubwa ya uwezo wake wa kijeshi katika maeneo mbalimbali ya mapambano; hatua ambayo wanadai imewezekana kufuatia kuimarika tena kwa mtiririko wa misaada ya kifedha kutoka Iran katika miezi ya karibuni.

Tel Aviv imeitaja hali hii kama kurudi kwenye kiwango cha zamani cha uwezo wa kuzuia vita kabla ya kuongezeka kwa mgogoro wa eneo, na ikaonya kuwa “kungojea bila kikomo” si chaguo tena - ishara ya uwezekano wa kupanuka kwa operesheni za kijeshi endapo njia za kidiplomasia hazitaleta matokeo ya wazi.

Ripoti hii imekuja wakati taasisi za usalama za Israel zinadai kuwa kiwango cha msaada wa Iran kwa Hezbollah, ambacho kilikuwa kimepungua kwa muda, kimeanza kuongezeka tena. Hali hii imeiwezesha Hezbollah kujenga upya mifumo yake ya makombora, mtandao wa uongozi na mawasiliano, na kuongeza uimara wa vikosi vyake maalumu, hususan kikosi cha Ridwan, katika maeneo ya kaskazini.

Katika ufichuzi mwingine, Yedioth Ahronoth imeandika, ikinukuu maafisa wa Tel Aviv, kwamba Lebanon imefanikiwa kuondoa silaha asilimia 80 katika maeneo ya kusini mwa Mto Litani. Israel inadai mafanikio hayo yametokana na shinikizo kubwa la kidiplomasia kwa ushirikiano na Washington, Paris na Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, maafisa hao walikiri kuwa serikali ya Lebanon haitaweza kukamilisha mchakato huo kabla ya mwisho wa mwaka kutokana na changamoto za kisiasa na kiusalama, pamoja na udhaifu wa serikali katika maeneo nyeti ya kusini.

Tathmini hizi zinakuja katika mazingira ambayo tangu Oktoba 2023, mpaka wa Lebanon–Israel umeshuhudia mashambuliano ya vipindi na kurushiana moto kwa kiwango kidogo, bila kufikia kiwango cha vita kamili. Wakati huohuo, Marekani, Ufaransa na wadau wengine wa kimataifa wanajaribu kuunda makubaliano ya hatua kwa hatua ili kuzuia kufanyika kwa vita vikubwa.

Kwa mujibu wa simulizi ya Israel, kurejea kwa uwezo wa kijeshi wa Hezbollah ni tishio la kimkakati ambalo halitaweza kudhibitiwa kwa diplomasia pekee — hususan kutokana na kuendelea kwa uzinduzi wa droni na makombora kuelekea maeneo ya kijeshi ya Jalili, na kuongezeka kwa shughuli za ulinzi za Hezbollah kaskazini mwa Litani.

Tahadhari hizi pia zimehusishwa na suala la utekelezaji wa Azimio 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Israel hudai kuwa azimio hilo linakataza uwepo wa wanamgambo wa Hezbollah kusini mwa Litani, ilhali Lebanon inasisitiza kuwa Israel yenyewe haijazingatia azimio hilo — haswa katika suala la kuondoka katika maeneo ya Shebaa Farms, kuachilia wafungwa wa Kilebanoni, na kusitisha mashambulizi ya kila siku ya anga.

Wataalamu wanakadiria kuwa matamshi haya ya maafisa wa Israel ni sehemu ya shinikizo la kisiasa kwa jumuiya ya kimataifa ili kuharakisha ufumbuzi wa mgogoro wa mpaka wa Lebanon, na kujaribu kuweka muundo mpya wa usalama utakaolisukuma jeshi la Hezbollah kurudi ndani zaidi ya ardhi ya Lebanon.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha